Kimataifa | Marekani kujiondoa rasmi makubaliano ya tabia nchi ya Paris

Na Asma Dady
Marekani imeanza rasmi mchakato wa kujitoa kutoka katika makubaliano ya Paris ya mazingira, kulingana na waziri wake wa mambo ya kigeni Mike Pompeo.

Rais wa  Marekani Donald Trump  alikuwa  mpinzani  mkubwa  wa makubaliano  hayo  wakati  alipokuwa  anawania  kiti  cha  urais, na utawala  wake  umekuwa  ukifanya  kila  unaloliweza kubadilisha sheria  za  mazingira, ukisema zinazuwia  biashara  na  kutoa  kwa nchi  nyingine  nguvu  ya  ushindani.

Pompeo alielezea  kuhusu kile  alichokiita "mzigo usio wa  haki wa kiuchumi uliowekwa  kwa  wafanyakazi wa  Marekani, biashara, na walipa  kodi, kwa  ahadi za Marekani  zilizotolewa  chini  ya makubaliano  hayo," wakati  akitangaza  kujitoa  huko. Amesema ,"mfano bora  na  wenye  uhalisia" utapendekezwa  na  Marekani kupinga  makubaliano  hayo  ya  dunia.

Makubaliano  ya  mwaka  2015 yalitiwa  saini  na  karibu  nchi  zote, na  kuuweka  utawala  wa  Trump  dhidi  ya  karibu  washirika  wake wote  pamoja  na  washindani  wake  wakuu  kuhusiana  na  suala  la mabadiliko  ya  tabia  nchi. Trump  binafsi  ni  mtu  mwenye  shaka na  mabadiliko  ya  tabia  nchi.

Utawala  wa  Trump rasmi uliuarifu  Umoja  wa  mataifa  hatua  yake hiyo  ya  kujitoa  siku ya Jumatatu, ukianza  mchakato  wa  mwaka mmoja  ambao  utakamilika  siku  moja  baada  ya  uchaguzi  wa  rais wa  Marekani  mwaka  2020.

Msemaji  wa  Umoja  wa  mataifa  alilithibitishia shirika  la  habari  la Ujerumani dpa kuwa  taasisi  hiyo  ya  dunia  imepokea  barua ya Marekani.

Credit:DW